Mama yangu alikuwa na jicho moja, nilikuwa namchukia sana, kwa ufupi
alikuwa kero sana kwangu. Mama alikuwa mpishi katika shule niliyokuwa
nasoma, ilikuwa ni shule iliyojengwa maalumu kwa ajili ya watoto yatima.
Pengine waweza kujiuliza kwa nini nilikuwa nasoma pale wakati nilikuwa
na wazazi? Ukweli ni kwamba baba yangu alikuwa amefariki
miaka mingi wakati mie bado mtoto mchanga. Mama aliomba kazi ya upishi
katika shule ile ili apate pesa za kunitunzia mimi wakati huo maana
baada ya kufariki baba ndugu walimpora mali zake zote na kumfukuza
katika nyumba yake, hivyo ndiyo sababu iliyopelekea mama kuomba kazi ya
upishi katika shule ile ili apate kujikimu kimaisha. Kama nilivyokwambia
hapo awali kwamba kutokana na jinsi alivyokuwa mama nilikuwa simpendi
kabisa. Mama yangu yeye alikuwa ananipenda sana na alijitahidi kunipenda
sana lakini sikujali hayo, kwani alikuwa ananikera sana na ile hali ya
kuwa na jicho moja.
Mama alikuwa ananitembelea kila mara
wakati wa mapumziko alikuwa akijisikia raha sana kuniona mwanae nikiwa
ana furaha wakati wote, lakini tofauti na hapo nilikuwa nakosa amani
sana kila alipokuwa akitokea tu. Basi mama wakati mwingine ilimbidi
asije kunisalimia maana alikuwa hapendi kuniudhi. Siku moja baada ya
juma moja kupita mama alikuja kunitembelea na kutaka kunijulia hali,
nilipomwaona tu nikakunja sura kuonyesha kukasirishwa na ule ujio wake.
Nikawaza moyoni mwangu na kusema “Hivi huyu mwanamke kwa nini
ananifanyia hivi?” ina maana yeye anajisikia raha kunikosesha amani.
Mama aliponiona tu alitabasamu na kunifuata ….. mmoja kati ya wanafunzi
wangu alicheka na kusema “ Eeeee muone mama yakooo ana jicho moja”
Maneno yale yalizidi kuongeza kichwani mwangu nilitamani ardhi ipasuke
niingie na inifunike. Na wakati mwingine nilitamani mama atoweke kabisa
nisimuone maishani mwangu. Mama aliposogea karibu yangu nilimtwanga
swali “Hivi wewe mwanamke unanipenda kweli?” mama yangu akajibu “Ndioo
mwanangu nakupenda sana tena zaidi ya sana kwani wewe ni mtoto wangu
pekee na sina mtoto mwingine zaidi yako, wewe ni lulu moyoni mwangu na
dhahabu machoni pangu na wewe ndio furaha ya maisha yangu” kwa hasira
huku nikifoka nikamwambia kama kweli unanipenda kwa nini usife ili mimi
nikawa na raha hapa duniani?. Mama yangu hakujibu kitu kwa wakati ule….
Akaamua kuondoka machoni pangu kimya kimya! Mimi wala sikuona kama lile
lilikuwa kosa na wala sikufikilia na wala sikupata walau hata nukta
moja ya kutafakari nini ninachokifanya, sababu nilikuwa nina hasira
sana. Ukweli nilikuwa sitambui mawazo yake mama na nilikuwa sijui nini
mama anavyowaza juu yangu. Na kwa vile sikuwa na lakumfanya kwa wakati
ule baada ya yeye kutoka mle ndani nami nikatoka nje huku nikiwa na
mawazo sana. Nilikuwa nasoma kwa bidii sana, na baada ya mtihani wa
mwisho nikapata bahati ya kuchaguliwa kuendelea na masomo ya juu jijini
Dar es salaam. Hivyo kwa nguvu ya shule nilisafirishwa kutoka Mbeya
mpaka dar, mama alinipatia pesa za matumizi pindi nitakapokuwa dar! Kwa
jinsi alivyokuwa ananipenda alinipa mshahara wake wa miezi mitano, kumbe
alikuwa ananitunzia hata kabla matokeo hayajatoka. Nilifurahi sana
ingawa sikumshukuru lakini mama hilo hakujali alifurahi sana vile
ambavyo nilipokea zile pesa kisha akanitakia safari njema. Nilipofika
dar nikaendelea na masomo yangu kama kawaida. Kwa bahati pia nikafauru
vizuri kisha nikaajiliwa Serikalini, Maisha yangu yalikuwa mazuri sana.
Nilijenga nyumba nzuri ya kifahari nikanunua gari ya kutembelea ilikuwa
gari aina ya Land cruzer mayai.
Sio siri maisha yangu yalikuwa
mazuri sana. Baadaye nikaamua kuoa mke, tukazaa watoto watatu, familia
yangu ilikuwa na furaha sana, sikuacha kuwasiliana na walimu wangu wa
mbeya katika ile shule ya watoto yatima niliyokuwa nikisoma hapo awali,
na kwa vile kwa wakati huo nilikuwa na pesa za kutosha nilikuwa natuma
misaada katika shule ile. Ila mama sikuwahi kutuma hata shilingi kumi.
Kwani nilikuwa natamani afe ili asiendelee kunitia aibu. Mama baada ya
kupata habari kuwa mwanae maisha yangu yamekuwa mazuri na pia alisikia
kuwa nimeoa na pia nimezaa watoto alifurahi sana na alitamani sana
kuwaona wajukuu zake. Kwa wakati huu mama yangu alikuwa ameanza kuzeeka
na aliamua kuacha kazi yake ya upishi katika ile shule. Pamoja na kuwa
alikuwa ni wanamke aliweza kujijengea kakibanda ka kujisitiri na kwa
vile alikuwa ameitumikia shule kwa muda mrefu hawakuacha kumtunza, pia
waliendelea kumpa mshahara wake kama kawaida maisha yakawa yanasonga.
Kwa upande wangu sikutaka hata kusikia habari zake. Siku moja mama
akaamua kunifuata Dar, ili walau awaone wajukuu zake na hata mie mwanaye
kwani alikuwa hajaniona zaidi ya miaka ishirini na mbili hivi, akapanda
basi na kuja dar kwa bahati alipofika dar alimpata msamalia mmoja
aliyeweza kumsitiri kama mjuavyo jiji la dar jinsi lilivyo na zamani
ilikuwa kutoka mbeya hadi dar unatumia siku mbili na kwa vile alikuwa
amefika usiku hakujua ni wapi aelekee.
Siku iliyofuata aliamua
kunitafuta kwa kuulizia na kwa vile mimi nilishakuwa mtu maarufu sana
hakupata shida kuipata nyumba yangu. Alipofika Getini alibisha hodi, na
mlinzi baada ya kumhoji na kupata maelezo alimruhusu aingie, alipokuwa
akikaribia mlango wangu, niliwasikia watoto wangu wakipiga kelele huku
wakimcheka mama yangu na kusema “Heee! Cheki hicho kibibi kizee chongo
kimekuja kwenye birthday party ya baba bila kualikwa” kusikia hivyo
nkatoka nje na nikamuona mama akija wakati huu alionyesha wazi kuwa
alikuwa mdhaifu! Ingawa hatukuonana kwa muda mrefu sana, sikuwa na hata
chembe ya kumkumbuka. Nilifoka na kumwambia “ We kizee wewe unathubutuje
kuja humu ndani na kuwashitua watoto wangu? Hauna hata haya tafadhari
sana naomba uondoke haraka hapa.” Tokaaa!! Mama aliniangalia kwa huruma
sana huku machozi yakimlengalenga katika macho yake, kisha akasema
“Samahani kijana wangu nimekosea nyumba aliyenielekeza alinielekeza
vibaya! Naomba unisamehe sana! Akageuka na kuanza kuondoka, haimaanishi
kuwa hakunitambua alifanya vile ili kuuridhisha moyo wangu!.. hivyo
akatoweka machoni pangu wala kuumia moyo kwa mama sikupata shida. Mama
alikwenda moja kwa moja stendi ya mabasi kukata ticketi ya kurudi mbeya.
Wakati ule ilikuwa manazi mmoja.
Akalala kwenye basi kesho
yake akaanza safari ya kurudi Mbeya. Siku moja nilipokea barua kutoka
katika ile shule niliyokuwa nikisoma ya watoto yatima, wakinihitaji
niende huko kulikuwa na sherehe iliyoandaliwa ya kuwakutanisha wanafunzi
wote waliosoma miaka ya nyuma ambao wamekuwa bega kwa bega katika
kuisaidia shule ile. Kwa hiyo hata mie nilikuwa mmoja wao, na kwa vile
nilijua kuwa nakwenda ni nyumbani sikutaka mke wangu amfahamu mama yangu
na pia sikutaka mke wangu ajue kuwa nilisoma shule ya watoto yatima
hivyo nikamuaga kuwa naenda Mbeya kikazi kwani siku zote mke wangu
nilimwambia kuwa mie ni mzaliwa wa Dar na sina ndugu kabisa wazazi wangu
wote wawili walifariki zamani sana. Siku iliyofuata nikaanza safari
yangu kuelekea nyumbani kwetu mbeya, wakati huu nilikuwa nawaza jinsi
ambavyo ningepokelewa kwa furaha pale shuleni lakini nilikuwa napata
shida sana kwamba naenda kukutana na mama yangu ambaye alikuwa kero sana
kwangu. Sikumpenda sana mama yangu hasa kwa lile tatizo lake la kuwa na
jicho moja. Nilifika salama mbeya na kwa vile nilikuwa nimetumia
usafiri wangu nilifika mapema kabisa, nikaenda katika moja ya nyumba za
kulala wageni iliyokuwa bora sana nyumba yenyewe ilikuwa ikiitwa Mount
Livingstone Hotel. Basi kama ilivyo ada nikaamka asubuhi na kujiandaa
tayari kwenda kwenye sherehe.
Nilipofika kwenye sherehe
kulikuwa na maclassmet kibao walikuwa wamefika pale na pia walikuwa na
wake zao na hata wale waliokuwa ni madada zetu walikuwa wamekuja na
waume zao, pamoja na hayo yote walikuwa wamekuja na wazazi wao karibu
kila mmoja alikuwa na mzazi japo mmoja. Kwa upande wangu nilikuwa peke
yangu, zaidi sana nilikuwa nimeambatana na dereva wangu tu. Lakini
halikunipa shida hilo na nilikuwa nimeshukuru sana mama yangu kutokuwepo
pale kwenye sherehe. Sio siri sherehe ilikuwa imefana sana na ilikuwa
ni ya aina yake. Baada ya sherehe tukaendelea kusalimiana na wale wazee
wa pale kijijini wote tukiwa na furaha sana. Baadaye akaja yule mama
aliyekuwa rafiki yake na mama yangu akaniambia “pole sana mwanangu kwa
msiba wa mama yako” Msiba wa mama? Nilimtwanga swali kuonekana kana
kwamba nimeshituka, ingawa nilijua wazi yule mama alikuwa anajua tabia
yangu na yale yote niliyokuwa nikimtendea mama yangu! Yule mama akasema
“ndioo mama yako alikufa mwezi week mbili zilizopita ina maana hukupata
taarifa? Nikamjibu sikupata taarifa. Basi tuakaendelea na mazungumzo
mengine, ila kusema ukweli ile taarifa ilinifurahisha moyoni mwangu
nikajua kuwa kero yangu sasa imekwisha. Hata hivyo mwisho wa mazungumzo
yule rafiki wa mama yangu aliniita pembeni na kuniomba niambatane naye
kwenda nyumbani kwake, nami bila hiyana nikakubali kwenda.
Tulipofika nyumbani kwake aliingia chumbani kwake na kutoka na barua
akanipatia ile barua na kuniambia kuwa mama yangu alisema anipatie
mimi….. Nilipokea ile barua kuanza kuisoma ilikuwa imeandikwa hivi:- Kwa
Mwanangu Kipenzi, Nimekuwa nikikuwazia wewe wakati wote, sababu
nakupenda sana, Naomba unisamehe sana kwa kuwatisha watoto wako siku ile
niliyokuwa nimekuja kwako Dar, naomba nisamehe sana mwanangu, nisamehe
sana. Nimepata furaha sana kusikia kuwa utakuja huku kwenye sherehe ya
shule yenu, lakini najua kuwa sitakuwepo kwenye sherehe hiyo, kwani
sipendi kukukwaza mwanangu. Ila mwanangu najua nimekukwaza kwa muda
mrefu lakini haikuwa malengo yangu ilikuwa ni kwa sababu ya upendo
niliokuwa nao kwako na vile nilivyopata tabu sana kukupata kwani wewe
ndiwe mtoto wangu wa pekee. Sikia mwanangu…… nataka ufahamu haya… Wakati
ukiwa angali bado mdogo ulipata ajali na kupoteza jicho lako moja na
mimi kama mama yako sikupenda kukuona mwanangu ukikua huku ukiwa na
jicho moja hivyo nikaamua kutoa jicho langu moja na kukuwekea wewe, ili
ukue huku ukifurahia ulimwengu huu mpya ukitumia kiungo changu ambalo
ndiyo jicho nililo kupatia. Nilikupenda sana mwanangu nab ado nakupenda
sana! Ni mimi mama yako!! Mwisho!.. NB: Ni stori tu ila kuna watu wana
tabia za kuwadharau wazazi hususani mama zao naomba kwa hali yoyote ile
mpende mama yako, hakuna aliye kama mama hapa Duniani!!! Nampenda sana
mama yangu
very nice story but also sad
ReplyDeleteStori nzuri inayoelimisha
ReplyDelete